Siku ya Mazingira Duniani: Miongo mitano ya hatua za kulinda mazingira

Tangu ilipozinduliwa mwaka wa 1974, Siku ya Mazingira Ulimwenguni imepanuka kuwa jukwaa la kimataifa la kuhamasisha na kushughulikia masuala nyeti kuanzia uchafuzi wa bahari na ongezeko la joto duniani hadi uhifadhi wa mazingira na uwindaji haramu. Mamilioni ya watu wameshiriki katika miaka iliyopita, hivyo kusaidia kubadilisha jinsi tunavyotumia rasilimali pamoja na kuchangia katika sera ya kitaifa na kimataifa ya mazingira. Yafuatayo ni baadhi ya matukio muhimu kuhusu Siku ya Mazingira Ulimwenguni katika miaka iliyopita.

Historia

Siku ya Mazingira Ulimwenguni imejumuisha mataifa madogo zaidi na yaliyoachwa nyuma kimaendeleo huku ikishughulikia mada nyeti zaidi: kuanzia uhifadhi wa mazingira hadi biashara haramu ya wanyamapori. Siku hii ya kuadhimishwa ulimwenguni kila mwaka iliyoanza zaidi ya miaka 40 iliyopita imevuma kwenye mitandao ya jamii.

2018

Maadhimisho ya 45 ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni yalifanyika nchini India na mada yake ilikuwa “Kukabiliana na Uchafuzi wa Plastiki.” Zaidi ya watu 6,000 walikusanyika kwenye Ufuo wa Versova mjini Mumbai kujumuika na mshindi wa tuzo la Bingwa wa Dunia wa Idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, Afroz Shah, kusafisha ufuo, ambapo walizoa zaidi ya kilo 90,000 za plastiki. Serikali ya India iliahidi kupiga marufuku plastiki zisizoweza kutumika upya— plastiki hizi huchangia asilimia 70 ya taka ya bahari—kufikia mwaka wa 2022 nao wabunge wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kuhusu amri ya kupiga marufuku itakayotekelezwa kufikia 2025.

2017

“Kuwaunganisha watu na mazingira”, ndiyo mada ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni 2017. Ilijumuisha zaidi ya matukio 1,800, kuanzia kupanda miti mjini Mumbai hadi kuchoma pembe nchini Angola na kukimbia kupita Mbuga ya Wanyama ya Iguaçu inayopatikana Brazili. Nchini Kanada ambako maadhimisho yalifanyika, Waziri Mkuu Justin Trudeau alijumuika na Erik Solheim wa idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa kufurahia mazingira kwa kuendesha kayaki kwenye Mto Niagara.

2016

Siku hii ilichochea kampeni ya #KuwalindaWanyamapori, kampeni kubwa zaidi kuwahi kufanywa mtandaoni na idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa na ilichangia pakubwa katika kukabiliana na uwindaji haramu kimataifa. Nchi ya Angola ambako maadhimisho yalifanyika iliahidi kukabiliana na biashara haramu ya pembe za ndovu. Kutokana na siku hii, China, mojawapo ya masoko makubwa ya bidhaa haramu za wanyapori, iliahidi kufunga masoko yake ya pembe za wanyamapori.

2015

Siku ya Mazingira Ulimwenguni ilivuma: maadhimisho yalifanyika Milan, Italia kauli mbiu yake ikiwa “Watu Bilioni Saba. Sayari Moja. Kuishi kwa Uwajibikaji,” hii ndiyo mada iliyovuma zaidi kwenye Twitter katika zaidi ya nchi 20; zaidi ya video 500 kuhusu Siku ya Mazingira Ulimwenguni zilichapishwa kwenye YouTube.

2014

Mada ya “Inua Sauti Yako Sio Bahari!” ilihamasisha kuhusu hatari zinazokabili mataifa yanayopatika kwenye visiwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Mwaka uliofuata, kwenye kikao cha Paris kuhusu hali ya hewa, mataifa madogo yanayopatikana kwenye visiwa yalitia saini mkataba wa kutimiza lengo la kukabiliana na ongezeko la joto kwa wastani wa digrii Selisiasi 1.5 kote duniani.

2013

Iliadhimishwa Mongolia, mada ya mwaka huu ilikuwa Fikiria.Kula.Hifadhi. Kampeni ilishughulikia kiwango kikubwa cha chakula kinachotupwa au kuharibika kila mwaka na ililenga kuwasaidia watu kufanya uamuzi wa busara ili kupunguza athari za uzalishaji chakula kwenye ikolojia.

Watu kote ulimwenguni walishiriki katika zaidi ya matukio 4,000 (mwaka wa 2011) na wakatembelea tovuti ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni zaidi ya mara milioni 4.25 (mwaka wa 2012); maadhimisho yalifanyika Uarabuni na Marekani kwa mara ya kwanza; ilipelekea suala la mabadiliko ya tabianchi kujadiliwa miaka mitatu mfululizo.

2012

Miaka ishirini baada ya Kongamano la Ulimwengu, maadhimisho ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni yalirejea Rio de Janeiro, Brazili. Mada ya “Uchumi Usioathiri Mazingira: Je, Unahusika?” ilihamasisha kuhusu Mpango wa Idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi Usioathiri Mazingira. Tovuti ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni ilitembelewa zaidi ya mara milioni 4.25, rekodi mpya.

2011

Shindano la kwanza la Siku ya Mazingira Ulimwenguni lilipelekea mwigizaji Don Cheadle kupata wafuasi zaidi mtandaoni kumliko Gisele Bündchen mwanamitindo mashuhuri, anayenuia kukuza msitu. Mwaka uliofuata, Gisele alipanda miti 50,000 kwenye Bustani ya Manispaa ya Grumari mjini Rio de Janeiro. Kote duniani watu walishiriki katika zaidi ya matukio 4,000.

2010

Mpango wa Kurithisha wa Siku ya Mazingira Ulimwenguni ulichangisha zaidi ya $85,000 zilizoelekezwa katika kuwalinda sokwe na utumiaji sola vijijini kote katika nchi mwenyeji ya Rwanda. Kwenye shindano la kimataifa mtandaoni wapiga kura waliwapa majina sokwe wachanga, wakiangazia hatari zinazowakabili kwenye sherehe ya Mwaka wa Ikolojia Ulimwenguni.

2007

Iliadhimishwa Tromsø, Norwe mada yake ikiwa “Barafu Inayeyuka? – Mada Nyeti”. Mwaka wa kwanza kati ya mitatu mfululizo ambapo siku hii iliibua mjadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kama ilivyobainika dhahiri kwenye Ripoti ya Nne ya Tathmini ya IPCC.

2006

Miaka kumi baada ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Umoja wa Kimataifa wa Kukabiliana na Kuenea kwa Jangwa, Siku ya Mazingira Ulimwenguni ilikuwa kikumbusho cha matatizo yanayokabili sehemu kame maadhimisho yalipofanyika Algiers, Aljeria kauli mbiu ikiwa “Jangwa na Kuenea kwa Jangwa – Tusieneze Jangwa kwenye Sehemu Kame!”

2005

Siku ya Mazingira Ulimwenguni aliadhimishwa Marekani Kaskazini kwa mara ya kwanza, mji wa San Francisco ukiwa mwenyeji wa mamia ya matukio mada ikiwa “Miji Isiyoathiri Mazingira: Mpango wa Sayari.” Mkataba wa Kyoto Protocol ulianza kutekelezwa na uzinduzi wake ukashuhudiwa na aliyekuwa Naibu wa Rais wa Marekani Al Gore na aliyekuwa Meya wa San Francisco Gavin Newsom.

2003

Maadhimisho yalifanyika Beirut, Lebanon, ya kwanza kabisa Uarabuni. Mada yake ya “Maji – Watu Bilioni Hawana ya Kutosha!” iliteuliwa kuunga mkono Mwaka wa Maji Safi Ulimwenguni.

Mataifa yaliyo na takriban thuluthi moja ya idadi ya watu duniani yakawa wenyeji wa Siku ya Mazingira Ulimwenguni, moja baada ya nyingine ikiwemo Uchina (mara mbili), Urusi, Japani na Uturuki; kampeni ikapelekwa mtandaoni.

river
MABADILIKO YA TABIANCHI, LIKIWEMO TISHIO LINALOKABILI MAENEO KAMA VILE MEKONG DELTA KUTOKANA NA KUINUKA KWA BAHARI, NDIYO MADA YA SIKU MAZINGIRA ULIMWENGUNI ILIYOSOMWA SANA.

2001

Katibu Mkuu Kofi Annan aliteua Siku ya Mazingira Ulimwenguni kuzindua kwa mara ya kwanza Utafiti wa Ikolojia wa Milenia, kutathmini afya ya sayari. Mada yake ikiwa “Jiunge kwenye Wavuti wa Maisha,” sherehe za kimataifa zilifanyika katika miji kadhaa: Torino, Italia na Havana, kuba na pia Hue, Vietnamu na Nairobi, Kenya.

2000

Idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa ilizindua tovuti kamili ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni, hivyo kuwawezesha watu kote duniani kuweka matukio yao na kukuza hisia ya jumuiya ya kimataifa. Maadhimisho yalifanyika Adelaide, Australia mada ikiwa “Milenia ya Mazingira – Ni Wakati wa Kuwajibika,” kabla ya kongamano la kimataifa lililobainisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia.

1998

Siku ya Mazingira Ulimwenguni iliangazia kwa mara ya kwanza matatizo yanayokumba ikolojia ya bahari, mada ikiwa “Dumisha Maisha kwa Kuokoa Bahari” ikiunga mkono Mwaka wa Bahari Ulimwenguni. Maadhimisho yalifanyika Moscow, Urusi.

1996

Mwanaharakati kutoka Naijeria Ken Saro-Wiwa alipokea tuzo ya Global 500 kwenye sherehe za WED mjini Ankara, Uturuki. Pamoja na zawadi, Siku ya Mazingira Ulimwenguni aliangazia uhusiano baina ya haki za binadamu na mazingira.

1995

Maadhimisho yalifanyika Afrika Kusini mwaka mmoja baada ya Nelson Mandela kutwaa urais. Mandela alihudhuria sherehe hizi, hivyo kuvuta nadhari za wengi duniani kuhusu mada za mazingira. Siku hii mwaka uliotangulia, kiongozi huyu wa vuguvugu dhidi ya ubaguzi wa rangi alitangaza Mlima wa Cape Town Ulio Tambarare kuwa “zawadi kwa Dunia” na ithibati ya juhudi za Afrika Kusini katika kulinda mazingira.

1993

Siku ya Mazingira Ulimwenguni iliadhimishwa Beijing, Uchina ikitoa hamasisho kuhusu mazingira katika nchi hii iliyo na watu wengi zaidi ulimwenguni, mada ikiwa “Umaskini na Mazingira – Kubadili Mitindo Iliyokolea.” Sherehe zitafanyika tena Uchina mwaka wa 2002, mjini Shenzen.

1992

Siku ya Mazingira Ulimwenguni iliadhimishwa mijni Rio de Janeiro, Brazili, wakati wa Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo, linalojulikana kama Kongamano la Dunia. Mataifa yalijadili mikataba muhimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kuenea kwa jangwa na ikolojia, na ikaweka mikakati ya maendeleo yanayozingatia uhifadhi wa rasilimali.

1989

Mwaka mmoja baada ya kubuniwa kwa Jopo la Mabadiliko ya Tabianchi Kati ya Serikali Mbalimbali, maadhimisho yalifanyika Brussels, Ubelgiji ambapo mada ilijumuisha ongezeko la joto duniani. Mada hii itajidiliwa tena mara nyingi zaidi kuliko mada zingine katika kampeni za baadaye za Siku ya Mazingira Ulimwenguni.

1988

Maadhimisho yalianza kufanyika katika sehemu tofauti duniani, kuanzia Bangkok, Tailandi. Mada ya “Watu Wanapotunza Mazingira, Maendeleo Hudumu” imekuja mwaka mmoja baada ya Ripoti ya Brundtland kutoa kiolezo chake chenye ushawishi kuhusu utunzaji.

1987

Idara ya Mazingira ya Umoja wa Mazingira iliadhimisha siku hii kwenye makao yake makuu mjini Nairobi, Kenya, kwa kutoa kwa mara ya kwanza tuzo za Global 500 kwa mabingwa wa mazingira akiwemo Wangari Maathai. Tuzo hizi zilisheheni maadhimisho ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni hadi mwaka wa 2003.

1986

Mada ya “Dumisha Amani Kwa Kupanda Mti” ilioana na Mwaka wa Amani Ulimwenguni. Kuonyesha jinsi Siku ya Mazingira Ulimwenguni inazidi kukua, viongozi wa kidini na kisiasa akiwemo Rais wa Ufaransa Francois Mitterand, Waziri Mkuu wa India Rajiv Gandhi na Rais wa Uganda Yoweri Museveni walishiriki katika “Sherehe ya Kimataifa” kwa kupanda miti na kuangazia uhusiano ulipo kati ya migogoro na uharibifu wa mazingira.

A tree for peace
ALIYEKUWA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA JAVIER PÉREZ DE CUÉLLAR AKIPANDA MTI KWENYE MAKAO MAKUU YA UMOJA WA MATAIFA MJINI NEW YORK SIKU YA MAZINGIRA ULIMWENGUNI MWAKA WA 1986.

Umoja wa Mataifa ulitenga tarehe 5 Juni kuwa Siku ya Mazingira Ulimwenguni mwaka wa 1972; miaka miwili baadaye, siku hii ilisherehekewa mara ya kwanza kauli mbiu ikiwa “Dunia Moja Pekee.”

1981

Kampeni iliangazia kemikali za sumu zinazopatikana katika maji yaliyo chini ya ardhi na mzunguko wa chakula. Mwaka uliofuata, Baraza Linaloongoza Idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa lilitwaa mpango wa Montevideo Programme, hivyo kupea kipaumbele utungaji sheria wa kimataifa unaopelekea makubaliano muhimu ya kimataifa kuzuia au kupiga marufuku vichafuzi au kemikali hatari.

1979

Mada ya “Njia Moja tu Kwa Watoto Wetu Kufikia Maisha ya Baadaye” ilioana na Mwaka wa Watoto Ulimwenguni. Kwa mara ya kwanza, Siku ya Mazingira Ulimwenguni iliangazia mwaka wa kimataifa uliotengwa na Umoja wa Mataifa, mtindo unaozidi kushuhudiwa kadri masuala ya mazingira yanavyozidi kuathiri dunia.

1977

Idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa ilichukua fursa hii kuangazia suala la ozoni, hivyo kuchochea Siku ya Mazingira Ulimwenguni kujadili mapema masuala nyeti yanayoathiri mazingira. Itachukua miaka kumi kufikia Mkataba wa Montreal Protocol kuhusu Mata Inayoharibu Ozoni.

1974

Siku ya Mazingira Ulimwenguni aliadhimishwa kwa mara ya kwanza kabisa kauli mbiu ikiwa “Dunia Moja Pekee.”

1972

Baraza Kuu la Umoja wa Maifa lilitenga tarehe 5 Juni kuwa Siku ya Mazingira Ulimwenguni, hivyo ikawa siku ya kwanza ya Kongamano la Stockholm kuhusu Mazingira. Pia liliafikia uamuzi wa kuanzisha Idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa siku hiyo.