Siku ya Mazingira Duniani: Miongo mitano ya hatua za kutunza mazingira

Tangu ilipozinduliwa mwaka wa 1974, Siku ya Mazingira Duniani imepanuka kuwa jukwaa la kimataifa la kuhamasisha na kushughulikia masuala nyeti kuanzia uchafuzi wa bahari na ongezeko la joto duniani hadi uhifadhi wa mazingira na uwindaji haramu. Mamilioni ya watu wameshiriki katika miaka iliyopita, hivyo kusaidia kubadilisha jinsi tunavyotumia rasilimali pamoja na kuchangia katika sera ya kitaifa na kimataifa ya mazingira. Yafuatayo ni baadhi ya matukio muhimu kuhusu Siku ya Mazingira Duniani katika miaka iliyopita.

Historia

Siku ya Mazingira Duniani imejumuisha mataifa madogo zaidi na yaliyoachwa nyuma kimaendeleo huku ikishughulikia mada nyeti zaidi: kuanzia uhifadhi wa mazingira hadi biashara haramu ya wanyamapori. Siku hii inayoadhimishwa ulimwenguni kila mwaka ilianza zaidi ya miaka 40 iliyopita na huvuma kwenye mitandao ya jamii.

2019

Kauli mbiu ya mwaka wa 2019 ilikuwa uchafuzi wa hewa, janga la kimataifa linalohitaji kushughulikiwa kwa dharura linalopelekea vifo vya mapema vya watu milioni 7 kutokea kila mwaka. Mwenyeji ikiwa Uchina, Rais Xi Jinping alisisitiza kujitolea kwa Uchina kushiriki tajriba yake na nchi nyinginezo kupitia kwa barua iliyosomwa wakati wa kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani ya mwaka wa 2019. Nchi hiyo pia ilizindua Ripoti ya Kuimarisha Ubora wa Hewa ya kipindi cha (2013–2018) ili kuonyesha sera zilizofaulu na kutafakari kuhusu mafunzo waliopata.

2018

Maadhimisho ya 45 ya Siku ya Mazingira Duniani yalifanyika nchini India chini ya kauli mbiu “Komesha Uchafu wa Plastiki.” Zaidi ya watu 6,000 walikusanyika kwenye Ufuo wa Versova mjini Mumbai kujumuika na Bingwa wa Dunia wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, Afroz Shah, kusafisha ufuo, ambapo walizoa zaidi ya kilo 90,000 za plastiki. Serikali ya India iliahidi kupiga marufuku plastiki zisizoweza kutumika upya— plastiki hizi huchangia asilimia 70 ya taka ya bahari—kufikia mwaka wa 2022 nao waunda sheria wa Muungano wa Ulaya walikubaliana kuhusu amri ya kupiga marufuku matumizi ya plastiki hizi itakayotekelezwa kufikia 2025.

2017

“Kuwaunganisha watu na mazingira”, ndiyo ilikuwa kauli mbiu ya Siku ya Mazingira Duniani iliyopelekea kutokea kwa shughuli zaidi ya 1,800 kama vile upandaji wa miti Mumbai, uchomaji wa pembe za ndovu nchini Angola, mashindano ya mbio katika Mbuga ya Kitaifa ya Iguaçu. Wenyeji wakiwa Canada, Waziri Mkuu Justin Trudeau aliungana na Mkurugenzi mtendaji wa UNEP, Erik Solheim kufurahia mazingira kwa kupiga kasia vyombo vya kayaks kwenye mto Niagara.

2016

Siku hiyo ilitumika kuzindua kampeni ya #WildforLife, kampeni kubwa ya kidijitali ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa iliyosaidia mno kukabiliana na uhalifu wa kimataifa dhidi ya wanyamapori. Nchi mwenyeji Angola iliahidi kukabiliana na biaashara ya pembe za ndovu. China, taifa linalopokea bidhaa kutokana na wanyamapori kinyume cha sheria, liliahidi kufunga soko lake ya pembe za ndovu.

2015

Siku ya Mazingira Duniani ilivuma: maadhimisho yalifanyika Milan, Italia kauli mbiu yake ikiwa “Watu Bilioni Saba. Sayari Moja. Kuishi kwa Uwajibikaji,” hii ndiyo mada iliyovuma zaidi kwenye Twitter katika zaidi ya nchi 20; zaidi ya video 500 kuhusu Siku ya Mazingira Duniani zilichapishwa kwenye YouTube.

2014

Kauli mbiu ya “Hamasisha Kuhusu Bahari, Usiibughudhi!” ilihamasisha kuhusu hatari zinazokabili mataifa yanayopatika kwenye visiwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Mwaka uliofuata, kwenye kikao cha Paris kuhusu hali ya hewa, mataifa madogo yanayopatikana kwenye visiwa yalitia saini mkataba wa kutimiza lengo la kukabiliana na ongezeko la joto kwa wastani wa nyuzijoto 1.5 kote duniani.

2013

Siku ya Mazingira Duniani iliadhimishwa Mongolia. Kauli mbiu ya mwaka wa 2013 ilikuwa Fikiria.Kula.Hifadhi. Kampeni hii ilishughulikia kiwango kikubwa cha chakula kinachotupwa au kuharibika kila mwaka na ililenga kuwasaidia watu kufanya uamuzi wa busara ili kupunguza athari kwenye ekolojia zinazotokana na uzalishaji chakula.

Watu kote ulimwenguni walishiriki katika zaidi ya matukio 4,000 (mwaka wa 2011) na wakatembelea tovuti Siku ya Mazingira Duniani zaidi ya mara milioni 4.25 (mwaka wa 2012). Maadhimisho yalifanyika Uarabuni na Marekani kwa mara ya kwanza; ilipelekea suala la mabadiliko ya tabianchi kujadiliwa miaka mitatu mfululizo.

2012

Miaka ishirini baada ya Kongamano la Ulimwengu, maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yalirejea Rio de Janeiro, Brazili. Kauli mbiu ya “Uchumi Usiochafua Mazingira: Je, Inakuhusu?” ilihamasisha kuhusu Programu ya Uchumi Usiochafua Mazingira ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa. Tovuti ya Siku ya Mazingira Duniani ilitembelewa zaidi ya mara milioni 4.25 ikiwa ni rekodi mpya.

2011

Shindano la kwanza la Siku ya Mazingira Duniani lilipelekea mwigizaji Don Cheadle kupata wafuasi zaidi mtandaoni kumliko Gisele Bündchen mwanamitindo mashuhuri, anayenuia kukuza msitu. Mwaka uliofuata, Gisele alipanda miti 50,000 kwenye Bustani ya Manispaa ya Grumari mjini Rio de Janeiro. Kote duniani watu walishiriki katika zaidi ya matukio 4,000.

2010

Mpango wa Kuridhisha wa Siku ya Mazingira Duniani ulichangisha zaidi ya dola za Marekani 85,000 zilizotumika kuwalinda sokwe na na kuweka mfumo wa umeme unatoumia nishati ya jua vijijini katika nchi mwenyeji ya Rwanda. Kwenye shindano la kimataifa mtandaoni wapiga kura waliwapa majina sokwe wachanga, wakiangazia hatari zinazowakabili kwenye sherehe ya Mwaka wa Bayoanuai Duniani.

2007

Iliadhimishwa Tromsø, Norwe chini ya kauli mbiu “Barafu Inayeyuka? – Mada Nyeti”. Mwaka wa kwanza kati ya mitatu mfululizo ambapo siku hii iliibua mjadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kama ilivyobainika dhahiri kwenye Ripoti ya Nne ya Tathmini ya IPCC.

2006

Muongo mmoja baada ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Kuenea kwa Jangwa, Siku ya Mazingira Duniani ilikuwa ukumbusho wa matatizo yanayokabili sehemu kame maadhimisho yaliyo fanyika Algiers, Aljeria kauli mbiu ikiwa “Jangwa na Kuenea kwa Jangwa – Tusieneze Jangwa kwenye Sehemu Kame!”

2005

Siku ya Mazingira Duniani aliadhimishwa Marekani Kaskazini kwa mara ya kwanza, katika mji wa San Francisco uliokuwa mwenyeji wa mamia ya shughuli chini ya kauli mbiu “Miji Isiyochafua Mazingira: Mpango wa Sayari.” Mkataba wa Kyoto ulianza kutekelezwa na uzinduzi wake ukashuhudiwa na aliyekuwa Naibu wa Rais wa Marekani Al Gore na aliyekuwa Meya wa San Francisco Gavin Newsom.

2003

Maadhimisho yalifanyika Beirut, Lebanon, yakiwa ya kwanza kabisa Uarabuni. Kauli mbiu ya “Maji – Watu Bilioni Hawana ya Kutosha!” Kauli mbiu hii ilichaguliwa kuunga mkono Mwaka wa Maji Safi Ulimwenguni.

Mataifa yaliyo na takriban thuluthi moja ya idadi ya watu duniani yakawa wenyeji wa Siku ya Mazingira Ulimwenguni, moja baada ya nyingine ikiwemo Uchina (mara mbili), Urusi, Japani na Uturuki; kampeni ikapelekwa mtandaoni kwa mara ya kwanza.

river
Mabadiliko ya tabianchi, likiwemo tishio linalokabili maeneo kama vile mekong delta kutokana na kuinuka kwa bahari, ndiyo mada ya siku mazingira ulimwenguni iliyosomwa sana.

2001

Katibu Mkuu Kofi Annan alichagua Siku ya Mazingira Duniani kuzindua kwa mara ya kwanza Utafiti wa Ikolojia wa Milenia, kutathmini hali ya sayari. Kauli mbiu ikiwa “Jiunge kwenye Wavuti wa Maisha,” sherehe za kimataifa zilifanyika katika miji kadhaa: Torino, Italia na Havana, kuba na pia Hue, Vietnam na Nairobi, Kenya.

2000

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa lilizindua tovuti kamili ya Siku ya Mazingira Duniani, hivyo kuwawezesha watu kote duniani kuzungumzia kuhusu shughuli zao na kuwazesha kufikia jamii ya kimataifa. Maadhimisho yalifanyika Adelaide, Australia kauli mbiu ikiwa “Milenia ya Mazingira – Ni Wakati wa Kuwajibika,” kabla ya kongamano la kimataifa lililobainisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia.

1998

Siku ya Mazingira Duniani iliangazia kwa mara ya kwanza matatizo yanayokumba ikolojia ya bahari, kauli mbiu ikiwa “Dumisha Maisha kwa Kuokoa Bahari” ikiunga mkono Mwaka wa Bahari Ulimwenguni. Maadhimisho yalifanyika Moscow, Urusi.

1996

Mwanaharakati kutoka Naijeria Ken Saro-Wiwa alipokea tuzo ya Global 500 kwenye sherehe za WED mjini Ankara, Uturuki. Pamoja na zawadi, Siku ya Mazingira Duniani aliangazia uhusiano baina ya haki za binadamu na mazingira.

1995

Maadhimisho yalifanyika Afrika Kusini mwaka mmoja baada ya Nelson Mandela kutwaa urais. Mandela alihudhuria sherehe hizi, hivyo kuvuta nadhari za wengi duniani kuhusu mada za mazingira. Siku hii mwaka uliotangulia, kiongozi huyu wa vuguvugu dhidi ya ubaguzi wa rangi alitangaza Mlima wa Cape Town Ulio Tambarare kuwa “zawadi kwa Dunia” na ithibati ya juhudi za Afrika Kusini katika kulinda mazingira.

1993

Siku ya Mazingira Duniani iliadhimishwa Beijing, Uchina ikitoa hamasisho kuhusu mazingira katika nchi hii iliyo na watu wengi zaidi ulimwenguni, kauli mbiu ikiwa “Umaskini na Mazingira – Kubadili Mitindo Iliyokolea.” Sherehe zilifanyika tena Uchina mwaka wa 2002, mjini Shenzen.

1992

Siku ya Mazingira Duniani iliadhimishwa mijni Rio de Janeiro, Brazili, wakati wa Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo, linalojulikana kama Kongamano la Dunia. Mataifa yalijadili mikataba muhimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kuenea kwa jangwa na ikolojia, na ikaweka mikakati ya maendeleo yanayozingatia uhifadhi wa rasilimali.

1989

Mwaka mmoja baada ya kubuniwa kwa Jopo la Mabadiliko ya Tabianchi Kati ya Serikali Mbalimbali, maadhimisho yalifanyika Brussels, Ubelgiji ambapo mada ilijumuisha ongezeko la joto duniani. Mada hii itajidiliwa tena mara nyingi zaidi kuliko mada zingine katika kampeni za baadaye za Siku ya Mazingira Duniani.

1988

Maadhimisho yalianza kufanyika katika maeneo mbalimbali duniani, kuanzia Bangkok, Tailandi. Kauli mbiu ya “Watu Wanapotunza Mazingira, Maendeleo Hudumu” ilikuja mwaka mmoja baada ya Ripoti ya Brundtland kutoa kielelezo chake chenye ushawishi kuhusu utunzaji.

1987

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa liliadhimisha siku hii kwenye makao yake makuu mjini Nairobi, Kenya, kwa kutoa kwa mara ya kwanza tuzo za Global 500 kwa mabingwa wa mazingira akiwemo Wangari Maathai. Tuzo hizi ziliendelea kutolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani hadi mwaka wa 2003.

1986

Kauli mbiu ya “Dumisha Amani Kwa Kupanda Mti” ilioana na Mwaka wa Amani Ulimwenguni. Kuonyesha jinsi Siku ya Mazingira Duniani inazidi kukua, viongozi wa kidini na kisiasa akiwemo Rais wa Ufaransa Francois Mitterand, Waziri Mkuu wa India Rajiv Gandhi na Rais wa Uganda Yoweri Museveni walishiriki katika “Sherehe ya Kimataifa” kwa kupanda miti na kuangazia uhusiano ulipo kati ya migogoro na uharibifu wa mazingira.

A tree for peace
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa javier pérez de cuéllar akipanda mti kwenye makao makuu ya umoja wa mataifa mjini new york siku ya mazingira duniani mwaka wa 1986.
 

Umoja wa Mataifa ulitenga tarehe 5 Juni kuwa Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 1972. Miaka miwili baadaye, siku hii ilisherehekewa mara ya kwanza kauli mbiu ikiwa “Dunia Moja Pekee.”

1981

Kampeni iliangazia kemikali za sumu zinazopatikana katika maji yaliyo chini ya ardhi na mzunguko wa chakula. Mwaka uliofuata, Baraza Linaloongoza Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa liliridhia mpango wa Montevideo Programme, hivyo kupea kipaumbele utungaji wa sheria za kimataifa unaopelekea makubaliano muhimu ya kimataifa kuzuia au kupiga marufuku vichafuzi au kemikali hatari.

1979

Kauli mbiu ya “Hatima Moja tu Kwa Watoto Wetu” ilioana na Mwaka wa Watoto Ulimwenguni. Kwa mara ya kwanza, Siku ya Mazingira Duniani iliangazia mwaka wa kimataifa uliotengwa na Umoja wa Mataifa, mtindo unaozidi kushuhudiwa kadri masuala ya mazingira yanavyozidi kuathiri dunia.

1977

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa lilichukua fursa hii kuangazia suala la ozoni, hivyo kuchochea Siku ya Mazingira Duniani kujadili mapema masuala nyeti yanayoathiri mazingira. Itachukua miaka kumi kufikia Mkataba wa Montreal Protocol kuhusu Mata Inayoharibu Ozoni.

1974

Siku ya Mazingira Duniani aliadhimishwa kwa mara ya kwanza kabisa kauli mbiu ikiwa “Dunia Moja Pekee.”

1972

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitenga tarehe 5 Juni kuwa Siku ya Mazingira Duniani, hivyo ikawa siku ya kwanza ya Kongamano la Stockholm kuhusu Mazingira. Pia liliafikia uamuzi wa kuanzisha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa siku hiyo.