Ukweli wa ajabu na mzuri kuhusu mifumo ya ekolojia ya nchi kavu  
Canva

Kampeni ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu inaangazia uboreshaji wa ardhi, kuenea kwa majangwa na kustahimili ukame chini ya kaulimbiu "Ardhi yetu. Mustakabali wetu. Sisi ni #GenerationRestoration.” Ukame na kuenea kwa majangwa kunatishia mifumo muhimu ya ekolojia katika sayari nzima, ikijumuisha mifumo ya ekolojia ya maji safi na udongo, viungo muhimu vinavyowezesha aina zote za maisha Duniani.

Hapa kuna mambo muhimu yanayofanya mifumo ya ekolojia ya nchi kavu na ardhi kuwa ya kipekee sana na, katika hali zingine, ya kutia moyo.

Udongo na maji 

  • Takriban asilimia 60 ya viumbe vyote huishi kwenye udongo, na hivyo kufanya ardhi kuwa makao ya viumbe hai wengi duniani. 
  • Udongo wenye rutuba huhifadhi kiasi kikubwa cha hewa ya ukaa, ambayo, ikiwa itaachiliwa, inaweza kusababisha ongezeko kubwa la joto duniani.
  • Asilimia 0.5 ya maji Duniani tu ni maji safi yanayoweza kutumika na kupatikana. Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri vibaya usambasaji wake. 
  • Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, hifadhi ya maji ardhini—ikiwa ni pamoja na unyevu wa udongo, theluji na barafu— imeshuka kwa kiwango cha sentimeta 1 kwa mwaka na kuwa na madhara makubwa kwa utoshelezaji wa maji na uzalishaji wa chakula.

Maeneo yaliokauka

  • Maeneo yaliokauka - eneo ambalo linakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji—linakalia asilimia 41 ya ardhi duniani na asilimia 78 ya maeneo ya malisho.
  • Maeneo yaliokauka huzalisha asilimia 44 ya mazao ya mimea duniani, ni chanzo cha chakula kwa nusu ya mifugo duniani na kusaidia maisha na kipato cha zaidi ya watu bilioni 2. 
  • Licha ya jina lake, nchi kavu ni makazi kwa zaidi ya robo ya misitu ya duniani, theluthi moja ya maeneo yabayoanuai duniani na ni maeneo muhimu kwa ndege wa kuhamahama.   

Majangwa

  • Majangwa hukalia zaidi ya humusi ya ardhi Duniani na hupatikana katika kila bara. 
  • Sahara ni jangwa kubwa zaidi la joto duniani, lina ukubwa wa kilomita mraba milioni 9.4, takribani ukubwa wa Canada.
  • Licha ya sifa yake ya kutokuwa na uhai, Jangwa la Sahara ni makazi kwa spishi 500 za mimea, spishi 70 za mamalia, spishi 100 za reptilia, spishi 90 za ndege, na athropoda kadhaa, kama vile buibui na nge. 
  • Majangwa mengi yanapanuka kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi lakini baadhi ya nchi zinapambana zikiwemo nchi 22 za Afrika zinazopakana na Jangwa la Sahara ambapo Ukuta Mkubwa wa Kijani unaolenga kurejesha hekta milioni 100 za ardhi kupitia mandhari ya kijani na inayozalisha mazao. 

Misitu

  • Misitu hukalia asilimia 31 ya Dunia lakini haijasambazwa kwa njia sawa kwani zaidi ya nusu ya misitu ya dunia inapatikana katika nchi tano pekee: Brazili, Kanada, Uchina, Shirikisho la Urusi na Marekani.
  • Misitu ni makazi kwa zaidi ya nusu ya spishi za juu za ardhi za wanyama, mimea na wadudu duniani.
  • Zaidi ya spishi 28,000 za mimea kwa sasa zimeripotiwa kutumiwa kama dawa na nyingi zinapatikana katika mifumo ya ekolojia ya misitu.
  • Vijidudu vya udongoni ni muhimu katika kuzalisha antibiotiki. Penicillin, kwa mfano, hutoka kwa kuvu wadogo wanaoishi kwenye udongo.
  • Kiumbe kikubwa zaidi duniani ni kuvu katika Milima ya Bluu ya Marekani. Inakalia takriban hekta 965 za ardhi, kuvu inaweza kuwa ya zamani kama miaka 8,650 hivi, hali inayoweza kuifanya kuwa kati ya viumbe hai vikongwe zaidi ulimwenguni. 

Maji safi

  • Maziwa, mito na ardhioevu hushikilia kati ya asilimia 20 hadi 30 duniani ya hewa ya ukaa licha ya kukalia asilimia kati ya 5 na 8 tu ya ardhi yake.
  • Mto Nile unachukuliwa kuwa njia ndefu zaidi ya maji duniani. Inaanzia Afrika Mashariki, inapita katika nchi 11 tofauti na ina urefu wa kilomita 6,695.
  • Takriban vipato bilioni 1.4 kote duniani vinategemea moja kwa moja uwepo wa maji safi, ikijumuisha kazi zinazohusiana na sekta za chakula na vinywaji, nishati na maji.

Mashamba

  • Kila sekunde tano, sawa na uwanja mmoja wa mpira wa miguu humomonyoka. Hata hivyo, inachukua miaka 1,000 kuzalisha sentimeta 3 za udongo wa juu ya ardhi.
  • Kila mwaka zaidi ya tani bilioni 24 za udongo wa juu ya ardhi wa thamani isiyojulikana husombwa na maji au kupeperushwa kote ulimwenguni, kwani ardhi inalimwa kupita kiasi na kulisha mifugo kupindukia na miti na misitu kukatwa. 
  • Ulimwengu utahitaji kuongeza uzalishaji wake wa chakula kwa asilimia kati ya 60 na 70 ili kulisha makadirio ya watu bilioni 9 kufikia mwaka wa 2050 hata kama upanuzi wa sasa wa kilimo unaendelea kutishia misitu na bayoanuai.
  • Takriban asilimia 75  ya mazao ya matunda na mbegu ulimwenguni hutegemea, angalau kwa kiasi, wachavushaji kama vile nyuki. Wachavushaji huchangia asilimia 35 ya jumla ya uzalishaji wa mazao duniani, na kuchavusha mazao 87 kati ya 115 ya chakula kikuu kote duniani.  
  • Licha ya umuhimu wao, wachavushaji wanadidimia mno,  hasa kutokana na mbinu za kilimo, matumizi ya viuatilifu, viumbe vamizi, magonjwa na mabadiliko ya tabianchi. 
  • Kote duniani, angalau watu bilioni 2 hutegemea sekta ya kilimo kwa kipato chao, hasa watu maskini na wa vijijini.

Miji

  • Miji hukalia chini ya asilimia moja ya ardhi Duniani, lakini ni makazi kwa zaidi ya nusu ya watu duniani. 
  • Miji huchangia asilimia 75 ya matumizi ya rasilimali na nishati duniani na kuzalisha zaidi ya nusu ya taka duniani na angalau asilimia 60 ya uzalishaji wa gesi ya ukaa. 
  • Zaidi ya thuluthi moja ya miji mikubwa, ikijumuisha Barcelona, ​​Bogota, New York na Tokyo, hupata sehemu kubwa ya maji yao ya kunywa ya hali ya juu kutoka kwa misitu iliyohifadhiwa iliyo karibu nao. 
  • Miti katika maeneo ya mijini inaweza kupunguza hewa angani kwa kiasi cha hadi nyuzijoto 5, na hivyo kupunguza mahitaji ya viyoyozi kwa asilimia 25. Miti mijini hutoa manufaa mengi ya kiafya kama vile maji safi. Pia husafisha hewa na kupunguza mafuriko mbali na manufa mengine mengi.