Siku ya Mazingira Duniani inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 5 mwezi wa Juni, huleta pamoja mamilioni ya watu kote duniani na kuwashirikisha kwenye jitihada za kutunza na kuboresha Dunia. Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 50 ya Siku ya Mazingira Duniani.
Jamii
Siku ya Mazingira Duniani ni jukwaa la kimataifa la kuchochea mabadiliko chanya. Watu kutoka kwa zaidi ya nchi 150 hushiriki katika siku hii ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa, ambayo inasherehekea hatua za kushughulikia mazingira na uwezo wa serikali, mashirika ya biashara na watu binafsi kuunda ulimwengu endelevu zaidi.
Hafla hii imekuwa likisimamiwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) tangu kuanzishwa kwake katika mwaka 1973.
Historia
Siku ya Mazingira Duniani huangazia changamoto kuu za mazingira tunazokumbana nazo kwa sasa duniani. Siku hii ya kimataifa ya umoja wa mataifa imepanuka na kuwa jukwaa kuu la kimataifa la kuhamasisha kuhusu mazingira huku mamilioni ya watu wakishiriki ili kutunza mazingira
2022 - Kuishi kwa amani na mazingira #DuniaMojaTu
Siku ya Mazingira Duniani iliangazia maadhimisho ya miaka 50 ya kile kinachochukuliwa kuwa mkutano wa kwanza wa kilele wa mazingira duniani, Mkutano wa mwaka wa 1972 wa Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira ya Binadamu. Kama desturi, ulitumia kaulimbiu "Dunia Moja Tu", ilioangazia umuhimu wa kutunza na kuboresha makazi ya pekee ya wanadamu.
Katika hafla rasmi ya mwaka wa 2022, nchi mwenyeji Uswidi iliahidi usitishaji wa kutoa leseni za uchimbaji upya wa makaa ya mawe, wa mafuta na gesi asilia. Zaidi ya watu milioni 65 walisherehekea Siku ya Mazingira Duniani mtandaoni.
2021 - Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia #GenerationRestoration
Siku hii iliangazia Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia chini ya kaulimbi “Tafakari. Buni. Boresha”. Mwenyeji akiwa Pakistan, iliangazia jinsi wanadamu wamekuwa wakitumia mifumo ya ekolojia ya sayari na kutoa wito kwa juhudi za pamoja za kimataifa kuchukuliwa ili kurekebisha uharibifu uliofanywa. Kila sekunde tatu, dunia hupoteza misitu mingi kiwango cha uwanja wa kuchezea mpira na katika karne moja iliyopita, nusu na maeneo oevu yameshaharibiwa.
2020 - Bayoanuai #TimeForNature
Katika mwaka wa 2020, Kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani iliangazia bayoanuai – suala lililopo linalopaswa kushughulikiwa kwa dharura. Nchi mwenyeji ilikuwa Kolombia. Kutokana na janga la COVID-19 – lililosababishwa na uharibifu wa kasi wa makaazi – Rais Iván Duque Márquez alisema "wakati wa kuchukua hatua ni sasa iwapo tunataka kuhakikisha kuwa kuna sasa na siku zijazo." Viongozi 14 duniani – ikijumuisha kutoka Costa Rica, Ufini, Ufaransa na Ushelisheli – walihutubia na kutoa wito kwa serikali kote duniani kuunga mkono lengo jipya la kimataifa la kutunza angalau asilimia 30 ya ardhi na bahari duniani kufikia mwaka wa 2030.
2019 -Uchafuzi wa hewa #KomeshaUchafuziWaHewa
Kaulimbiu ya mwaka wa 2019 ilikuwa uchafuzi wa hewa, janga la kimataifa linalohitaji kushughulikiwa kwa dharura linalopelekea vifo vya mapema vya watu milioni 7 kutokea kila mwaka. Mwenyeji ikiwa Uchina, Rais Xi Jinping alisisitiza kujitolea kwa nchi yake kushiriki tajriba yake ya kukabiliana na uchafuzi wa hewa na mataifa mengine. Uchina ilizindua Ripoti ya Kuimarisha Ubora wa Hewa ya kipindi cha (2013–2018) ili kuonyesha sera zilizofaulu na kutafakari kuhusu mafunzo waliopata.
2018 - Komesha uchafuzi wa plastiki #KomeshaUchafuziWaPlastiki
India ilikuwa mwenyeji wa maadhimisho ya 45 ya Siku ya Mazingira Duniani chini ya kaulimbiu “Komesha Uchafuzi wa Plastiki.” Zaidi ya watu 6,000 walikusanyika kwenye Ufuo wa Versova mjini Mumbai kujumuika na Bingwa wa Dunia wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, Afroz Shah, kusafisha ufuo, ambapo walizoa zaidi ya kilo 90,000 za plastiki. Serikali ya India iliahidi kupiga marufuku plastiki zisizoweza kutumika zaidi ya mara moja— plastiki hizi huchangia asilimia 70 ya taka ya baharini—kufikia mwaka wa 2022 watunga sheria wa Muungano wa Ulaya walikubaliana kuhusu marufuku itakayotekelezwa kufikia mwaka wa 2025.
2017 - Kuunganisha watu na mazingira #imwithnature
“Naungana na mazingira”, ndiyo ilikuwa kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani katika mwaka wa 2017, iliyopelekea kutokea kwa hafla zaidi ya 1,800 kama vile upandaji wa miti mjini Mumbai, uchomaji wa pembe za ndovu nchini Angola na mashindano ya mbio katika Mbuga ya Kitaifa ya Iguaçu nchini Brazil. Mwenyeji akiwa Canada, Waziri Mkuu Justin Trudeau aliungana na Erik Solheim wa UNEP kuungana na mazingira kwa kupiga kasia vyombo vya kayaks kwenye mto Niagara.
2016 - Biashara haramu ya wanyamapori #WildforLife
Siku hiyo ilitumika kuzindua kampeni ya #WildforLife, kampeni kubwa ya kidijitali ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa kwa wakati huo iliyosaidia mno kukabiliana na uhalifu wa kimataifa dhidi ya wanyamapori. Nchi mwenyeji Angola iliahidi kukabiliana na biashara ya pembe za ndovu. Uchina, taifa linalopokea bidhaa kutokana na wanyamapori kinyume cha sheria, pia liliahidi kufunga soko lake ya pembe za ndovu.
2015 - Utumiaji mzuri wa rasilimali na matumizi na uzalishaji endelevu wa bidhaa #ConsumewithCare
Siku ya Mazingira Duniani ilivuma. Maadhimisho yalifanyika Milan, Italia kauli mbiu ikiwa “Watu Bilioni Saba. Sayari Moja. Tumia kwa Njia ya Kuwajibika,” hii ndiyo mada inayovuma zaidi kwenye Twitter katika zaidi ya nchi 20.
2014 - Nchi Ngogo za Visiwa na Mabadiliko ya Tabianchi #MabadilikoYaTabianchi
Kaulimbiu ya “Hamasisha Kuhusu Bahari, Usiibughudhi!” ilihamasisha kuhusu hatari zinazokabili mataifa yanayopatika kwenye visiwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Mwaka uliofuata, kwenye kikao cha Paris kuhusu hali ya hewa, mataifa madogo yanayopatikana kwenye visiwa yalifikia makubaliano ya kutimiza lengo kabambe la kukudhibiti ongezeko la joto lisizidi wastani wa nyuzijoto 1.5 kote duniani.
2013 - Tafakari.Kula.Okoa. Punguza Athari yako #ThinkEatSave
Siku ya Mazingira Duniani iliadhimishwa Mongolia, kaulimbiu ikiwa “Tafakari.Kula.Okoa.” Kampeni hii ilishughulikia athari za kiwango kikubwa cha chakula kinachotupwa kwa mazingira na kusaidia watu kufanya uamuzi wa busara wai kupunguza athari za kiekolojia zinazotokana na uzalishaji chakula.
2012 - Uchumi Usiochafua Mazingira : Unakujumuisha? #DoesItIncludeYou?
Miaka ishirini baada ya Mkutano wa Kilele wa Dunia, maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yalirejea Rio de Janeiro, nchini Brazili. Kaulimbiu ya “Uchumi Usiochafua Mazingira: Je, Unakujumuisha?” ilihamasisha kuhusu juhudi za UNEP za kubuni mfumo wa fedha endelevu zaidi duniani. Tovuti ya Siku ya Mazingira Duniani ilitembelewa zaidi ya mara milioni 4.25 ikiwa ni rekodi mpya.
2011 - Misitu: Mazingira Hukuhudumia
Siku ya Mazingira Duniani ilijumuisha Shindano la kirafiki kati ya mwigizaji Don Cheadle na Mjasiriamali Gisele Bündchen kutafuta kuona ni nani anaweza kuvutia wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii. Kama sehemu ya shindano, Gisele alipanda miti 50,000 kwenye Bustani ya Manispaa ya Grumari mjini Rio de Janeiro. Kote duniani watu walisajili shughuli zaidi ya 4,000 kuhusiana na Siku ya Mazingira Duniani.
2010 - Hatima Moja
Mpango wa Kuridhisha wa Siku ya Mazingira Duniani ulichangisha zaidi ya dola za Marekani 85,000 zilizotumika kuwalinda sokwe na kuweka mfumo wa umeme unatoumia nishati ya jua vijijini katika nchi mwenyeji ya Rwanda. Kwenye shindano la kimataifa mtandaoni wapiga kura waliwapa majina sokwe wachanga, wakiangazia hatari zinazowakabili katika Mwaka wa Bayoanuai Duniani.
2009 - Sayari Yako Inakuhitaji: Shirikiana Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi
2008 - Achana na Mazoea! Kuwa na Uchumi wa Kiwango Kidogo cha Gesi ya Ukaa
2007 - Barafu Inayeyuka - Mada Nyeti?
Chini ya kaulimbiu “Barafu Inayeyuka? – Mada Nyeti” iliadhimishwa mjini Tromsø, nchini Norwe. Ulikuwa mwaka wa kwanza kati ya mitatu mfululizo ambapo siku hii iliangazia mabadiliko ya tabianchi. Inatokea baada ya Ripoti ya Nne ya Tathmini ya Jopo la Serikali Mbalimbali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi naobainisa kuwa ongezeko la joto ni hali ya kutiliwa shaka.
2006 - Majangwa na Kuenea kwa Majangwa – Usieneze Majangwa kwenye Maeneo Kame!
Muongo mmoja baada ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Kuenea kwa Majangwa, Siku ya Mazingira Duniani ni ukumbusho wa matatizo yanayokabili sehemu kame wakati maadhimisho yalipofanyika nchini Aljeria chini ya kaulimbiu “Majangwa na Kuenea kwa Majangwa – Tusieneze Jangwa kwenye Sehemu Kame!”
2005 - Majiji yasiochafua Mazingira: Pangia Sayari!
Siku ya Mazingira Duniani iliadhimishwa Marekani Kaskazini kwa mara ya kwanza, katika mji wa San Francisco uliokuwa mwenyeji wa mamia ya shughuli chini ya kaulimbiu “Miji Isiyochafua Mazingira: Mpango wa Sayari.” Siku iliyoadhimishwa wakati Mkataba wa Kyoto ulpoanza kutekelezwa, hafla hii ilishikisha aliyekuwa Naibu wa Rais wa Marekani Al Gore na aliyekuwa Meya wa San Francisco Gavin Newsom.
2004 - Inahitajika! Bahari - Marehemu au Hai?
2003 - Maji: Watu Billion Mbili Wanakufa Kuyapata!
Maadhimisho rasmi yalifanyika mjini Beirut, nchini Lebanon, yakiwa ya kwanza kabisa Asia Magharibi. Kaulimbiu ya “Maji – Watu Bilioni Hawana ya Kutosha!” ilichaguliwa kuunga mkono Mwaka wa Kimataifa wa Maji Safi.
2002 - Toa Fursa kwa Dunia
2001 - Ungana na Mtandao wa Maisha Ulimwenguni
Maadhimisho yaliandaliwa na Italia. Katibu Mkuu Kofi Annan alichagua Siku ya Mazingira Duniani kuzindua Tathmini ya Mifumo ya Ekolojia ya Milenia, juhudi za kipekee za kutathmini hali ya sayari. Kauli mbiu ikiwa “Jiunge kwenye Wavuti wa Maisha Duniani,” sherehe za kimataifa zilifanyika katika miji kadhaa: Torino, Italalia; Havana, Cuba; Hue, Viet Nam; na Nairobi, Kenya.
2000 - Milenia ya Mazingira-- Ni Wakati wa Kuchukua Hatua
Maadhimisho yaliandaliwa na New Zealand. UNEP yazindua tovuti kamili ya Siku ya Mazingira Duniani, hivyo kurahisishia watu kote duniani kusajili shughuli zao na kuwazesha kufikia jamii ya kimataifa. Maadhimisho rasmi yalifanyika Adelaide, Australia kaulimbiu ikiwa “Milenia ya Mazingira – Ni Wakati wa Kuwajibika,” kabla ya kongamano la kimataifa lililobainisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia.
1998
Siku ya Mazingira Duniani iliangazia kwa mara ya kwanza matatizo yanayokumba ekolojia ya bahari, kauli mbiu ikiwa “Dumisha Maisha Duniani kwa Kuokoa Bahari” ikiunga mkono Mwaka wa Bahari Ulimwenguni. Maadhimisho yalifanyika mjini Moscow, Urusi.
1996
Mwanaharakati kutoka Nigeria Ken Saro-Wiwa alipokea tuzo ya Global 500 kwenye sherehe za Siku ya Mazingira Duniani mjini Ankara, Uturuki. Pamoja na tuzo hii, Siku ya Mazingira Duniani iliangazia uhusiano baina ya haki za binadamu na mazingira.
1995
Maadhimisho yalifanyika Afrika Kusini mwaka mmoja baada ya Nelson Mandela kutwaa urais. Mandela alihudhuria sherehe hizi, hivyo kuvuta nadhari za wengi duniani kuhusu mada za mazingira. Siku hii mwaka uliotangulia, kiongozi huyu wa vuguvugu dhidi ya ubaguzi wa rangi alitangaza Mlima wa Cape Town Ulio Tambarare kuwa “zawadi kwa Dunia” na ithibati ya juhudi za Afrika Kusini za kutunza mazingira.
1993
Siku ya Mazingira Duniani iliadhimishwa Beijing, Uchina ikihamasisha kuhusu mazingira katika nchi hii iliyo na watu wengi zaidi ulimwenguni, kauli mbiu ikiwa “Umaskini na Mazingira – Kubadili Mitindo Mibaya Iliopo.” Sherehe zilifanyika tena Uchina mwaka wa 2002, mjini Shenzen.
1992
Siku ya Mazingira Duniani iliadhimishwa mijni Rio de Janeiro, Brazili, wakati wa Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo, maarufu kama Mkutano wa Kilele wa Dunia. Mataifa yalijadili kuhusu mikataba muhimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kuenea kwa majangwa na baayoanuai, na ikaweka mikakati ya kisasa ya maendeleo endelevu.
1989
Mwaka mmoja baada ya kubuniwa kwa Jopo la Mabadiliko ya Tabianchi Kati ya Serikali Mbalimbali, maadhimisho yalifanyika mjini Brussels, Ubelgiji yakiangazia suala la ongezeko la joto duniani. Kaulimbiu hii itajidiliwa tena mara nyingi zaidi kuliko kaulimbiu nyingine katika kampeni za baadaye za Siku ya Mazingira Duniani.
1988
Maadhimisho rasmi yalianza kufanyika katika maeneo mbalimbali duniani, kuanzia mjini Bangkok, Tailandi. Kaulimbiu ya “Watu Wanapotanguliza Mazingira, Maendeleo Hudumu” ilikuja mwaka mmoja baada ya Ripoti ya Brundtland kutoa kielelezo chake chenye ushawishi kuhusu uendelevu.
1987
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa liliadhimisha siku hii kwenye makao yake makuu mjini Nairobi, Kenya, kwa kutoa kwa mara ya kwanza tuzo za Global 500 kwa mabingwa wa mazingira akiwemo Wangari Maathai. Tuzo hizi ziliendelea kutolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani hadi mwaka wa 2003.
1986
Kaulimbiu ya “Dumisha Amani Kwa Kupanda Mti” ilioana na Mwaka wa Amani Ulimwenguni. Kuonyesha jinsi Siku ya Mazingira Duniani inavyozidi kukua, viongozi wa kidini na kisiasa akiwemo Rais wa Ufaransa Francois Mitterand, Waziri Mkuu wa India Rajiv Gandhi na Rais wa Uganda Yoweri Museveni walishiriki katika maadhhimisho ya Kimataifa kwa kupanda miti na kuangazia uhusiano ulipo kati ya mizozo na uharibifu wa mazingira.
1981
Kampeni iliangazia kemikali za sumu zinazopatikana katika maji yaliyo chini ya ardhi na kwenye mifumo ya usambasaji wa chakula. Mwaka uliofuata, Baraza Linaloongoza Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa liliridhia mpango wa Montevideo, hivyo kutoa kipaumbele kwa utungaji wa sheria za kimataifa zinazopelekea makubaliano muhimu ya kimataifa ya kuzuia au kupiga marufuku vichafuzi au kemikali hatari.
1979
Kaulimbiu ya “Hatima Moja tu Kwa Watoto Wetu” ilioana na Mwaka wa Watoto Ulimwenguni. Kwa mara ya kwanza, Siku ya Mazingira Duniani iliangazia mwaka wa kimataifa uliotengwa na Umoja wa Mataifa, mtindo unaozidi kushuhudiwa kadri masuala ya mazingira yanavyozidi kuathiri dunia.
1977
UNEP ilitumia fursa hii kuangazia suala la tambiko la ozoni, hivyo kuchochea Siku ya Mazingira Duniani kujatoa mwelekeo mapema wa kushughulikia masuala nyeti yanayoathiri mazingira. Itachukua miaka kumi kufikia Mkataba wa Montreal kuhusu Vitu Vinayoharibu Tambiko la Ozoni.
1973
Siku ya Mazingira Duniani aliadhimishwa kwa mara ya kwanza kabisa kaulimbiu ikiwa “Dunia Moja Tu.”
1972
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitenga tarehe 5 Juni kuwa Siku ya Mazingira Duniani, hivyo ikawa siku ya kwanza ya Kongamano la Stockholm kuhusu Mazingira ya Binadamu. Azimio lingine, lililopitishwa na Baraza Kuu siku hiyo, lilipelekea kuanzishwa kwa UNEP.